Koti
kuva: L. Packalen
Binafsi

Sewangi 6.6.2002

Wapendwa wetu wa Suomi, Pokeeni salam za upendo toka Tanzania. Ni matumaini yetu kwamba nyote hamjambo na mnaburudika na majira ya kiangazi.

Wapendwa, imepita miezi mitano sasa tangu tuliporejea nyumbani kutoka huko Suomi. Tunapenda kuwafahamisha kuwa sisi hatujambo na tunafurahia maisha ya nyumbani. Mara tu baada ya kurejea hapa nyumbani tulikuwa na hofu kubwa ya kuugua malaria. Hata hivyo, tulikuta dawa ya vyandarua inayoitwa NGAO ambayo huua na kufukuza mbu kabisa. Tumekuwa tukitumia dawa hiyo na bila shaka imetusaidia tusipate malaria mpaka sasa kwani chandarua hutukinga kabisa dhidi ya mbu wa malaria. Dawa ya NGAO hupatikana katika vidonge na huuzwa kwenye maduka karibu yote ya dawa. Kidonge kimoja huuzwa kwa bei ya shilingi mia nne tu za Tanzania (sawa na Euro 0.5). Chandarua kilichofuliwa kwenye maji yaliyotiwa kidonge kimoja cha NGAO hufukuza mbu kwa muda wa miezi minne. Kwa bahati nzuri vyandarua vinapatikana kwa wingi hapa Tanzania na kwa bei ndogo kabisa kwani havilipiwi ushuru wowote serikalini. Yasemekana kwamba matumizi ya vyandarua vyenye dawa ya NGAO yamepunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi ya maleria hasa kwa watoto wadogo. Kwetu sisi hizi ni habari njema na tungependa kuwashauri kwamba mtakapotembelea Tanzania muhakikishe kuwa mnalala ndani ya vyandarua vyenye dawa ya NGAO ili mjilinde na malaria.

Wapendwa, katika kipindi cha miezi mitano iliyopita tangu turejee hapa nyumbani, tumeshuhudia mtukio mbalimbali yakiwemo ya hali ya hewa, siasa, uchumi na majanga. Tumeona ni vyema tuwape taarifa fupi juu ya baadhi ya matukio hayo. Ni matumaini yetu kwamba mtafurahi kuzisoma taarifa hizo.

Matukio ya hali ya hewa yanahusu mvua. Mwanzoni mwa Aprili, sehemu mbalimbali za Tanzania zilipata mvua kubwa na za kutisha. Mvua hizo zilisababisha hasara mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuangusha nyumba na kubomoa madaraja. Daraja la mto Mkwazu huko katika barabara ya Chalinze-Segera lilivunjika na kusababisha kukatika kwa mawasiliano baina ya jiji la Dar na mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, na Arusha kwa siku kadhaa. Katika tukio hilo gari moja lilitumbukia katika daraja lililovunjika na kuua watu watatu. Huko mkoani Morogoro, maji yaliyojaa katika mito yalisababisha kuzama kwa kivuko katika mto Kilombero na kuua watu tisa. Kivuko hicho kilikuwa kikitoka wilaya ya Ulanga kwenda wilaya ya Kilombero. Hata hivyo sasa hivi mvua hizo zimepungua kabisa na watu wameanza kuvuna mazao yao mashambani.

Matukio ya uchumi yaliyotawala katika kipindi hiki ni yale ya matayarisho ya kubinafsishwa kwa shirika la umeme (TANESCO) na shirika la reli. Kwa upande wa shirika la umeme, tumeshuhudia kupanda ghafla kwa gharama za umeme hivi karibuni. Kupanda huko kulisababisha kilio kikubwa kutoka kwa watumiaji wa umeme na kwa wanamazingira. Wakati huohuo, menejimenti ya shirika la umeme ilichukuliwa na wasimamizi kutoka Afrika ya kusini ambao wataliongoza shirika hilo hadi litakapobinafsishwa. Kwa upende wa shirika la reli, mipango inaendelea ya kupunguza wafanyakazi kabla shirika hilo halijabinafsishwa rasmi. Shirika lingine ambalo nalo liko mbioni kubinafsishwa ni lile la Mamlaka ya maji mijini ambalo kwa mji wa Dar es Salaam hufahamika kama DAWASA. Wananchi wameyapokea matukio haya kwa hisia tofauti. Wapo wananch wanakubali mabadiliko hayo kwa matumaini kuwa yataongeza ubora wa huduma za umeme, maji na usafiri wa treni, ambazo kwa sasa haziridhishi kabisa. Kwa upande mwingine, wapo ambao hawayakubali mabadiliko hayo kwa sababu yanapelekea watu wengi kupoteza kazi zao wakati huu ambao ni vigumu kabisa kupata kazi nyingine.

Kwa upende wa siasa, tumeshuhudia raisi Benjamin Mkapa akikubali kukutana kwa mara ya kwanza na viongozi wa vyama vya upinzani. Mpaka sasa amekutana na Bwana Makani wa chama cha CHADEMA, Profesa Lipumba wa chama cha CUF, Bwana Mbatia wa chama cha NCCR-Mageuzi, na Bwana Cheyo wa chama cha UDP. Kiongozi wa chama cha TLP, Bwana Mrema bado hajapata nafasi ya kukutana na raisi. Katika mikutano yao na raisi, viongozi wa vyama vya upinzani wameshauriana na raisi juu ya mambo mbalimbli yakiwemo ya kikatiba, na ya kiuchumi. Watanzania wengi wemaeipokea hatua hiyo ya raisi kama mwanzo mwema wa kuimarisha demokrasia ya vyama vingi katika nchi.

Tukio jingine la kisiasa linahusu kugawanywa kwa mkoa wa Arusha katika mikoa miwili ya Manyara na Arusha. Mkoa wa Manyara una wilaya za Babati, Hanang, Kiteto, Simanjiro na Manyara. Nao mkoa wa Arusha una wilaya za Arumeru, Arusha, Karatu, Monduli, na Ngorongoro.

Huko Zanzibar nako tumeshuhudia mabadiliko ya nane ya Katiba ya Zanzibar ambayo yamefanywa ili kuboresha mazingira ya demokrasia ya vyama vingi. Mabadiliko hayo yanaruhusu kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi ambayo itakuwa na wajumbe kutoka katika vyama mbalimbali vya siasa. Aidha mabadiliko hayo yanawapa wafungwa haki ya kupiga kura wawapo magerezani. Mabadiliko haya yanachukuliwa na watu wengi kama mtokeo ya muafaka uliofikiwa hivi karibuni baini ya vyama vya CCM na CUF.

Kwa upande wa majanga, tumeshuhudia janga la moto ambao uliteketeza ubalozi wa Kenya na kituo cha Redio Claud FM. Moto huo ambao ulitokea usiku wa Jumatano ya tarehe 10.5.02, uliunguza ofisi mbalimbali kaitka ghorofa nne za juu kabisa za jengo la Kitegauchumi ambalo lina jumla ya ghorofa 14. Katika miaka ya nyuma kidogo ofisi ya Ubalozi wa Suomi ilikuwa katika jengo hilo. Inasemekana kwamba moto huo ulilipuka kutokana na hitilafu ya umeme.

Hivi karibuni kabisa, tarehe 17 Mei, tumeshuhudia ajali mbaya kabisa ya barabarani ambapo basi la abiria kutoka Songea kuja Dar es Salaam lilipinduka huko katika milima ya Lukumburu na kuua jumla ya watu 37. Watu walionusurika katika ajali hiyo mbaya ni watu watano tu. Kulingana na picha za ajali hiyo tulizozishuhudia kwenye televisheni, kichwa cha dereva wa gari hilo kilikatika na kutengana na kiwiliwili. Ajali hiyo ilihuzunisha sana watu hapa.

Watanzania ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu walipatwa na msiba mkubwa wa kuondokewa na Shekhe wao mkuu Hemed Bin Jumaa bin Hemed aliyefariki mwanzoni mwa mwezi wa tano na kuzikwa huko kwao Tanga. Kwa mujibu wa magazeti, Shekhe Hemed bin Jumaa bin Hemed alizaliwa mwaka 1928 huko Tanga. Wakati wa uhai wake, Shekhe Hemed bin Jumaa bin Hemed alipigania sana upatanisho na upendo miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali. Juhudi hizo zilimfanya apendwe na Wtanzania wote wasiopenda migogoro baina ya kidini mbalimbali.

Wapendwa wetu wa Suomi, kwa ufupi ni hayo tu kwa leo. Kwa kumalizia tungependa kumshukuru sana Bwana Leif Packalen kwa kututembelea nyumbani kwetu Mbezi Msigani, Dar es Salaam. Tulifurahi sana kukutana naye tena tukiwa nyumbani kwetu na kukaa pamoja kuanzia saa kumi hadi saa moja na nusu jioni. Bila shaka wapendwa wengine mtatutembelea pale mtakapofika Tanzania. Karibuni sana.

Sewangi & Felister.
University of Dar es Salaam
Box 35110
Dar es Salaam
Tanzania
Sewangi@hotmail.com

Downage -_-

Sivujen toteutus: Joonas From (voxel(at)mbnet.fi) ja päivitys: Andrea Fichtmüller, 2007. Suomi-Tansania seura on koonnut tämän sivuston tiedot eri lähteistä eikä vastaa niiden paikkansapitävyydestä.