Koti
kuva: L. Packalen
Mvua

Sewangi 6.10.2003

Barua Kutoka Dar

Wapendwa wetu wa Suomi,

Kwa mara nyingine tunawakumbuka kwa salamu za upendo kutoka Dar. Kwa mbali tunawaona mkianza kutafakari juu ya makoti na buti zenu za baridi kama ishara ya kukaribisha tena majira ya baridi kali na giza.

Wapendwa wetu, huku Dar tunaendelea vyema na tupo katika kipindi cha jua na tayari joto limeanza. Kwa jumla hali ya uoto wa nchi haipendezi sana kutokana na kiangazi cha muda mrefu kidogo. Hali ya chakula sio nzuri pia kwani katika baadhi ya maeneo tayari kuna upungufu mkubwa wa chakula kiasi kwaamba Serikali imeanza kugawa chakula cha msaada katika maeneo hayo. Mategemeo ya wakulima wengi sasa yapo katika mvua fupi za vuli ambazo zinatarajiwa kuanza mwezi huu wa kumi. Hali ya chakula mijini pia sio nzuri hasa katika jiji la Dar es Salaam lenye zaidi ya milioni tatu. Bei za baadhi ya vyakula, hasa mahindi, mchele na maharage, zimepanda karibu mara mbili na kuna uhaba mkubwa wa matunda. Baada ya kuwajulisha hali ilivyo kwa upande wa hali ya hewa, sasa tuwafahamishe mambo kadhaa yaliyotokea hapa kwetu tangu tulipowaletea barua yetu ya mwisho.

Kwa upande wa siasa, tulipata ugeni mzito wa Raisi Mwai Kibaki wa Kenya. Rais Kibaki alitembelea Tanzania tarehe 23 Juni, ikiwa ni ziara yake ya kwanza kabisa tangu alipochanguliwa kwa kishindo kuwa raisi wa Kenya mwishoni kabisa mwa mwaka jana. Ziara hiyo ilijaa shamrashamra na shangwe nyingi hasa wakati wa mapokezi ambapo chama tawala pamoja na vyama vya upinzani vilijitokeza kumlaki na kumpongeza kwa ushindi wake huo ambao ulimwondoa Mzee Moi katika kiti cha uraisi alichokikalia kwa muda mrefu.

Jambo lingine lililojiri katika medani za siasa na kuvuta masikio ya wengi lilikuwa ni kuibuka kwa mjadala juu ya dhana ya ‘Uzawa’. Mjadala huu uliibuliwa na Mbuge wa Ilala (CCM), Mheshimiwa Idi Simba kwa kuandika kijitabu kilichopembua falsafa yake ya Uzawa na nafasi ya Mzawa katika zama hizi za utandawazi wa kubinafsisha na kugenisha uchumi. Katika mjadala huo Chama cha Mapinduzi kilimkana Mbunge wake huyo kwa kusisitiza kuwa hakihusiki kabisa na falsafa ya Uzawa na kilipiga marufuku matumizi ya msamiati huo katika shughuli zake zote. Hatua hii ilichukuliwa kwa kuchelea kuwa dhana hiyo kama ilivyo inaweza kupanda mbegu ya ubaguzi na hata ukabila kwa msingi wa mahali watu walikozaliwa. Badala yake chama hicho kilisisitiza kuwa msingi wa dira yake ni Uzalendo na wala sio uzawa. Vipo vyama vya upinzani ambavyo vinashikilia kwamba katika hali ya mambo ya sasa ambapo wenyeji wanatupwa pembezoni katika maswala ya ubinafsishaji na ugenishaji uchumi, dhana ya Uzwa haiwezi kuepukika. Hivyo dhana hii, japo imekataliwa na CCM bado inatumiwa na vyama hivyo.

Kwa upande wa uchumi yametokea mambo kadhaa. Moja lililoshangiliwa sana na Watanzania ni lile la kufutwa kwa kodi iliyokuwa imebatizwa kwa jina ‘kodi ya maendeleo’ Kodi hiyo ilikuwa kero kubwa kwa watanzania wengi masikini wa vijijini kiasi cha kuwafanya baadhi yao wazihame kaya zao na kwenda kuishi porini ambako wasingeweza kukamatwa na kudaiwa ama hata kufungwa kwa kutolipa kodi . Kodi hiyo ilitupiliwa mbali katika bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2003/2004 iliyowasilishwa bungeni mwezi Juni na waziri wa Fedha, Mheshimiwa Basili Pesambili Mramba. Pamoja na kodi hiyo, zilifutwe pia kodi nyingine nyingi ikiwemo ada ya ndoa na ya mitihani. Aidha katika bajeti hiyo kodi za simu za mkononi (‘kanyuka’ kwa kutohoa kwenye Kifini) zilipunguzwa kwa kiwango cha asilimia 5 hadi 7. Pamoja na hayo yote ni kutokuwepo kwa kodi ya kuingiza kompyuta na vifaa vyake pamoja na vitabu vya masomo. Kutokuwepo kwa kodi hizi ni motisha kubwa ya maendeleo ya nchi yetu katika teknolojia ya habari na mawasiliano na katika elimu kwa jumla.

Tukio jingine kubwa la kiuchumi lililovuta masikio ya Watanzania wengi ni kuzinduliwa kwa daraja la kisasa la mto Rufiji. Daraja hilo kubwa la aina yake lina urefu wa mita 970.5 na upana wa mita 10.8, na lilijengwa kwa msaada mkubwa kutoka Mfuko wa Misaada wa Kuwait (Kuwait Fund). Kuzinduliwa kwa daraja hilo ambalo limesilimishwa kwa jina la ‘Daraja la Mkapa’, kumerahisisha sana usafiri wa barabara wa kwenda mikoa ya Lindi na Mtwara. Hali hiyo inatarajiwa kufungua neema ya kiuchumi katika mikoa hiyo na kutokomeza lindi la umaskini lililotanda humo kwa muda mrefu.

Tukio jingine lilikuwa ni lile la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuikatia Zanzibar umeme kwa muda wa masaa matatu hapo tarehe 21 Julai 2003. Jambo hili ambalo lilizua tafrani baina ya Shirika na Serikali ya Zanzibar, lilitokea bila kutarajiwa na wengi. Hata hivyo lilitoa funzo muhimu kwa Serikali na taasisi zake kuwa enzi zile za kutumia umeme bila kulipa hazipo tena baada ya kampuni hiyo kugenishwa na kuanza kufanya kazi kwa misingi ya kibishara badala ya ile ya kisiasa.

Kwa upande wa vijambo vya maisha, Mzee Malecela alipata jiko baada ya muda mrefu wa kuishi maisha ya upweke yaliyomkuta kutokana na kifo cha mkewe miaka kadhaa iliyopita. Mzee huyo wa kuheshimika ambaye pia ni Mbunge wa Mtera (CCM) na Makamu Mwenyekiti wa Chama tawala (CCM) alifunga ndoa ya Kikristo na mbunge wa viti maalum (CCM) Bi. Anne Kilango.

Nao wapenzi wa kinywaji, hususan bia , wa jiji la Dar, wenye tabia ya kuvinjari baa hadi usiku wa manane walipatwa na simanzi kubwa baada ya Mkuu wa Mkoa, Mzee Yusuf Makamba kuifufua sheria ya kufunga Baa zote saa tano kamili usiku. Yasemekana sheria hiyo ni ya muda mrefu ila tu ilikuwa haitekelezwi hali ambayo iliwafanya baadhi ya wanywaji kuhamia baa hadi usiku wa manane. Mzee Makamba, ambaye ametokea kuwa maarufu sana kutokana na jitihada zake za kutatua matatizo ya wakazi wa jiji, aliifufua sheria hiyo kama njia ya kupambana na wimbi la ujambazi ulioshamiri jijini. Kabla ya hapo baadhi ya majambazi walijichimbia kwenye mabaa wakinywa hadi usiku wa manane walipokwenda kufanya uharamia wao kwa wananchi. Kulingana na sheria hii yeyote atakayekutwa akinywa pombe Baa baada ya saa tano usiku atakamatwa pamoja na mwenye Baa. Hata hivyo kadri siku zinavyopita ndivyo utekelezaji wa sheria hiyo iliyofufuliwa unavyozidi kufifia.

Ndugu zetu wa Suomi tunamalizia barua hii kwa kuwatakia moyo wa matumaini mnapoingia kwenye majira magumu ya baridi kali na giza yaliyo mbele yenu. Pia kama kawaida yetu tunapenda kuwashukuru wale wote waliotutembelea hapa Dar na hasa nyumbani kwetu Mbezi Msingani. Tunamshukuru sana rafiki yetu Traute Stude ambaye alitutembelea nyumbani kwetu na kukaa nasi kwa siku nzima. Pia tunamshukuru bwana Anoldi Chiwalala ambaye alitutembelea na kuandamana nasi hadi Bagamoyo kutembelea Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo pamoja na vivutio vingine vilivyoko humo. Tunamshukuru pia bwana Bonanza kwa kutupigia simu alipokuwa Dar japo tulishindwa kuonana kutokana na kazi nyingi zilizokuwa zimemkabili. Mwisho tunamshukuru sana Bwana Mshana kwa salamu zake kwetu na kwa Usharika wetu wa Mbezi Luis.

Karibu Dar, Karibu Mbezi Msigani.

Ni sisi wapendwa wenu

Sewangi & Felister
Box 35110, Dar.
Puh. 0744.821137

Downage -_-

Sivujen toteutus: Joonas From (voxel(at)mbnet.fi) ja päivitys: Andrea Fichtmüller, 2007. Suomi-Tansania seura on koonnut tämän sivuston tiedot eri lähteistä eikä vastaa niiden paikkansapitävyydestä.