Koti
kuva: L. Packalen
Ukimwi

Sewangi 5.11.2002

Barua Kutoka Dar

Wapendwa wetu wa Suomi

Pokeeni salamu zetu toka Dar. Tunawasalimu tukitumaini kuwa nyote hamjambo na mnaendea kuchapa kaza baada ya mapumziko ya majira ya joto. Tunapenda kuwafahamisha kuwa huku tunaendelea kuchapa kazi na hatujambo kabisa. Tunawatumia waraka huu ili tuwajulishe, walau kwa ufupi, baadhi ya mambo ambayo yametokea huku kwetu Tanzania katika kipindi cha miezi mitano tangu tulipowatumia waraka wetu wa nyuma.

Tukianza na upande wa hali ya hewa na uchumi, hapa sasa ni kipindi cha mvua za vuli katika maeneo ambayo hupata mvua hizo. Kwa jumla hali ya hewa ni nzuri na hatutarajii kupata matatizo ya ukame kama ilivyotokea huko katika nchi za Malawi, Zambia, Zimbabwe na Msumbiji. Kutokana na hali hiyo nzuri ya hewa, hali ya chakula ni ya kuridhisha na bei ni za kawaida. Hivi karibuni, wakulima wa mahindi wa mikoa ya Mbeya, Rukwa na Ruvuma wamepata bei nzuri ya mahindi yao kutokana na mahitaji makubwa ya mahindi huko Malawi, Jamhuri ya Kongo, na Zambia. Kwa upande wa mazao ya biashara, hali ya wakulima bado sio nzuri kwani bei ya mazao kama vile korosho, pamba, na kahawa bado ziko chini sana. Kilo moja ya kahawa imeshuka hadi wastani wa shilingi ya Tanzania 350/ ambayo ni karibu sawa na Euro 0.35! Ukilinganisha bei hii na bei ya kikombe kimoja cha kahawa hapo Suomi utagundua kuwa dunia hii ‘iliyostaarabika’ ina maajabu yake.

Tarehe 13 Juni, ilikuwa siku ya bajeti ya Tanzania. Bajeti hiyo iliyosomwa na waziri wa fedha, Mheshimiwa Mramba, ilikuwa na mambo mengi yenye kutia matumaini. Moja kati ya hayo ambayo tumeona ni vyema tuwadokezee ni kuwa kodi ya ushuru kwa kompyuta na vifaa vyake imeondolewa. Hivyo sasa hivi utakapotembelea Tanzania usisite kubeba kompyuta yako kwani hakuna ushuru wa forodha. Serikali imeamua kufanya hivyo ili kuchochea matumizi ya kompyuta miongoni mwa wananchi na hasa vyuoni na mashuleni.

Kwa upande wa maisha, tumeshuhudia matukio ya hapa na pale mengi yakiwa ni ya kuhuzunisha na kutisha kidogo. Tarehe 24 Juni, 2002, watanzania tuligubikwa na huzuni kubwa kutokana na ajali mbaya ya treni ya abiria iliyotokea huko Dodoma na kusababisha vifo vya watanzania 281. Treni iliyopata ajali iliondoka Dar. siku ya Jumapili, 23/7/02 jioni kuelekea Kigoma na Mwanza. Asubuhi ya siku iliyofuata, Jumatatu, ajali ilitokea baada ya treni kushindwa kupanda mlima na kuanza kurudi nyuma kwa kasi ya ajabu. Mwendo huo wa kasi wa kurudi nyuma ulichukua kama dakika 30 hivi hadi treni hiyo ilipogonga treni nyingine ya mizigo kwa kishindo kikubwa na kusababisha baadhi ya mabehewa kurushwa juu na kutupwa mbali kabisa na njia ya reli. Mabehewa mengi yaliyoanguka yalikuwa ya daraja la tatu ambayo kwa kawaida hujaza sana abiria. Katika ajali hiyo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilipoteza jumla ya wanafunzi watatu na wengine kadhaa walijeruhiwa. Wanafunzi waliopatwa na ajali hiyo walikuwa wanakwenda kwenye mazoezi kwa vitendo. Katika jumla ya watu 281 waliopoteza maisha yao, 193 walitambuliwa na ndugu zao na 88 hawakutambuliwa, hivyo walizikwa na Serikali.

Katika mwezi huohuo wa Juni, kiasi cha wachimba madini wadogowadogo zaidi ya 40 walipoteza maisha yao huko Mererani, Arusha, baada ya kuvuta hewa chafu ndani ya migodi. Aidha, wananchi wawili walipoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea huko Bariadi, Mwanza. Tetemeko hilo liliacha watu wengi bila nyumba baada ya kuangusha jumla ya nyumba 1326. Eneo lililopatwa na tetemeko liko ndani ya bonde la ufa kandokando mwa ziwa Victoria. Kwa kawaida eneo hilo kupatwa na matetemeko ya ardhi ya mara kwa mara.

Sensa ya nane, tangu Tanzania ipate uhuru, ilianza tarehe 25/8/02. Kabla ya uhuru, sensa ya kwanza ilifanyika Tanganyika mwaka 1913, ambapo idadi ya watu wakati huo ilikuwa milioni 4.1. Mwaka 1931 Sensa ya pili ilifanyika na Tanganyika ilikuwa na watu milioni 5.29. Sensa ya kwanza baada ya uhuru ilifanyika mwaka 1967. Wakati huo Tanzania ilikuwa na watu milioni 12. Sensa ya pili baada ya uhuru ilikuwa mwaka 1978 ambapo idadi ya Watanzania ilifikia milioni 18. Katika sensa ya tatu, mwaka 1988, jumla ya watanzania ilikuwa milioni 23. Sasa hivi inakadiriwa kuwa jumla ya Watanzania ni milioni 33.

Tukio jingine la kuhuzunisha lilitupata tarehe 28/8/02 ambapo mwanamuziki chipukizi na machachari, James Dandu, alitutoka ghafla. Jemes Dandu ambaye alifahamika sana kama ‘Cool Jemes’ au ‘Mtoto wa Dandu’ alifariki dunia usiku wa tarehe 28, kutokana na ajali ya gari iliyotokea eneo la kijiji cha Makumbusho, Mwenge, majira ya saa tano na nusu usiku. Msanii huyo chipukizi ambaye alianza fani hiyo ya muziki akiwa Sweden alirejea Tanzania mwanzoni mwa mwaka huu. Katika jitihada zake za kukuza muziki wa Tanzania, Mtoto wa Dandu aliaanzisha tuzo ya muziki ya ‘Kilimanjaro Music Award’ kwa ajili ya wasanii wa Tanzania. Kifo cha James kilitokea wakati akiwa amekamilisha kurekodi albamu yake ya 12 tangu aanze muziki. Dandu ameacha mke, Devotha Chuwa, na watoto wawili, Caroline (8) na Michael (6).

Kwa upande wa maswala ya Afya, Watanzania wenye maradhi ya UKIMWI wataanza kupata dawa ya kurefusha maisha. Dawa hiyo aina ya Fluconazole inayotengenezwa na kampuni ya Pfizer ya Marekani, ilizinduliwa mwezi wa nane, mjini Dar. Kwa mujibu wa waziri wa Afya, mama Anna Abdalla, dawa hiyo itakuwa ikitolewa bure kwa wagonjwa wote mahospitalini. Gharama za dawa hiyo kwa mgonjwa mmoja ni jumla ya shilingi za Tanzania 100,000 kwa mwezi. Kutolewa bure kwa dawa hii kutawawezesha wagonjwa wote wanaostahili waipate bila matatizo.

Siku ya Nyerere. Serikali ya Tanzania imeamua kuwa kuanzia mwaka huu, tarehe 14 Oktoba ya kila mwaka itakuwa sikukuui ya kumbukumbu ya Baba wa taifa, Mwalimu J.K. Nyerere aliyefariki Oktoba 14, 1999. Siku hiyo itafahamika kama ‘Siku ya Nyerere’.

Wapendwa wetu wa Suomi, yapo mengi ambayo yametokea huku, lakini haitawezekana kuyaeleza yote katika waraka huu wetu mfupi. Hata hivyo kabla ya kuufunga waraka huu, tunapenda kuwapa Wasuomi wote pole zetu za dhati kwa tukio la bomu lililolopuka katika kituo cha Myyrmanni. Tuliposoma habari za tukio hilo katika mtandao wa Intaneti hatukuamini. Ilituchukua muda kabla hatujatambua kwamba kweli bomu limelipuka huko Suomi. Hakika tulishtuka sana kwa vile, miaka mitano ya maisha yetu Suomi ilitufanya tuamini kuwa Suomi ni pepo ya amani isiyo na mabomu ya magaidi. Hata hivyo tulifarijika tuliposikia kuwa bomu hilo halikuwa la magaidi bali lilitokana na mwanafunzi mmoja, baradhuli, aliyependa tu kuchezea mabomu bila kujali kwamba alikuwa akihatarisha maisha yake na ya Wasuomi wenzake. Poleni sana kwa hofu na mshtuko mlioupata kutokana na tukio hilo.

Mwisho tungependa kuwashukuru sana Daktari Tapio Pitkanen na Mchungaji Sirkka Peltola kwa kututembelea nyumbani kwetu, Mbezi Msigani, wakati walipokuwa hapa Tanzania mwezi wa Septemba. Ni matumaini yetu kuwa nanyi wengine mtakapofika Tanzania mtatutembelea. Karibuni sana.

Tunawatakia nguvu na matumaini katika kipindi hiki kigumu cha majira ya giza na baridi.

Sewangi & Felister
University of Dar es Salaam
Box 35110
Dar es Salaam (TZ)
Puh. 0744 821137

Downage -_-

Sivujen toteutus: Joonas From (voxel(at)mbnet.fi) ja päivitys: Andrea Fichtmüller, 2007. Suomi-Tansania seura on koonnut tämän sivuston tiedot eri lähteistä eikä vastaa niiden paikkansapitävyydestä.