Koti
kuva: L. Packalen
Money

Sewangi 30.1.2003:

Barua Kutoda Dar

Wapendwa wetu wa Suomi,

Tunawasalimu nyote kwa kuwatakia HERI YA MWKA MPYA WA 2003 na kwa kuwapa pole ya baridi kali katika majira haya ya baridi na giza.

Kwa mara nyingine tena tunawatumia waraka wetu huu mfupi ili tuweze kuwafahamisha baadhi ya mambo ya huku kwetu. Kwa vile ndio tu tumeingia katika mwaka mpya wa 2003, tumeamua kwamba katika waraka huu tuwape tathmini fupi na ya jumla juu ya hali ya mambo ilivyokuwa hapa kwetu katika mwaka uliomalizika wa 2002.

Kwa mtazamo wa jumla kabisa, mambo mengi ya mwaka wa 2002 yalikuwa ya kawaida hasa tukizingatia kwamba hapakuwa na mabadiliko yoyote ya kimwelekeo. Hata hivyo tukienda ndani kidogo, tunaweza kusema kwamba mambo ya mwaka wa 2002 yalikuwa na sura mbili: sura ya matumaini na sura ya kukatisha tamaa.

Tukiana na upande wa uchumi, juhudi za serikali za kukarabati na kujenga miundo mbinu mipya hasa barabara zilikuwa za kutia matumaini. Kwa mfano, ujenzi wa daraja kubwa na la aina yake katika mto Rufiji umewatia matumaini makubwa wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi. Daraja hilo limewahakikishia usafiri wa uhakika kutoka wa kwenda katika mikoa ya kaskazini ukiwemo mkoa maarufu wa Dar es Salaam. Aidha kufunguliwa kwa soko la kisasa la samaki kule Magogoni kumekuwa faraja kubwa kwa wachuuzi wa samaki kwani sasa lile tatizo la kusumbuliwa na mvua wakati wa biashara limemalizika. Kwa upande wa pili, wananchi wamekatishwa tamaa na kushuka kwa kasi kiwango cha ajira na kwa bei za mazao ya wakulima.. Kinyume kabisa na matarajio ya wengi, zoezi la ubinafsishaji na uuzaji wa viwanda na mashirika limesababisha upungufu mkubwa wa ajira hasa kwa vijana. Hali hii imepelekea kuongezeka kwa kasi kwa vitendo vya wizi na ujambazi hasa katika maeneo ya mijini kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wakazi wa mijini wasio na kazi. Nao uuzaji huria wa mazao ya wakulima umesababisha kushuka sana kwa bei ya mazao hayo. Hali hii imepelekea kushuka kwa kasi kabisa kwa kiwango cha maisha huko vijijini.

Kwa upande wa siasa, Muafaka uliofikiwa baina ya vyama vya CCM na CUF ulifungua sura ya matumaini ya amani hasa katika visiwa vya Zanzibar. Ule uhasama uliokuwepo baina ya wafuasi wa vyama hivi umepungua kwa kiasi kikubwa, hali ambayo inaashiria matumaini ya amani ya kudumu. Aidha wananchi wengi wamepata matumaini mapya ya kuimarika kwa demokrasia ya vyama vingi kutokana na uamuzi wa Raisi wa kukutana na Viongozi wa vyama vya siasa visivyo madarakani. Hata hivyo kwa upande wa pili mizozo ndani ya vyama vya siasa imekuwa jambo ka kukatisha tamaa kwa wananchi ambao wangependa kuviona vyama hivyo vikiimarika na kuwa na ushindani wa kweli wa kisiasa.

Katika michezo, kauli ya Serikali kwamba itajenga uwanja wa kisasa kabisa wa kandanda badala ya ule mkongwe wa Taifa imekuwa ni ya matumaini makubwa kwa wananchi hasa kwa wapenzi wa kandana. Kwa upande mwingine matokeo mabaya ya timu zetu katika michezo ya kimataifa yalikatisha tamaa. Mwaka wa 2002 haukuwa mzuri kimichezo kwa maana kwamba timu za Tanzania zilifanya vibaya sana katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Kwa upande wa elimu, kauli ya Serikali ya kufuta kabisa ada kwa elimu ya msingi ilitoa matumaini makubwa kwa wananchi, hasa kwa wasiokuwa na uwezo kifedha, kuwa watoto wao wangepata elimu ya msingi. Hata hivyo hali ya upungufu mkubwa wa majengo, waalimu na vitabu kwa ajili ya elimu ya msingi, hasa katika sehemu za vijijini, ilikatisha tamaa. Shule nyingi zilikuwa na wanafunzi wengi pasipo waalimu wala vitabu wala majengo ya kutosha.

Kwa upande wa afya ya jamii, hali ya kukatisha tamaa ilitokana wingi wa vifo vilivyotokana na magonjwa wa UKIMWI na Malaria. Hata hivyo matumizi ya vyandarua vilivyotiwa dawa ya NGAO yameleta matumaini kidogo katika mapambano dhidi ya malaria. Kwa upande wa UKIMWI, Serikali iliwapa wagonjwa matumaini kwamba ahadi yake ya kuwa itakuwa ikiwapatia bure wagonjwa dawa za kurefusha maisha na za kuzuia uambukizo kwa watoto wanaozaliwa na mama walioathirika.

Upande uliokatisha tamaa zaidi ulikuwa ule wa ajali mbalimbali zilizotokea katika mwaka wa 2002 na kusababisha kupotea kwa mali nyingi na maisha ya watu. Ajali za barabarani zilikuwa nyingi kiasi cha kutisha na kukatisha tamaa. Ajali ya treni ya abiria iliyotokea huko Dodoma ilikuwa mbaya kuliko zote zilizowahi kutokea katika historia ya usafiri wa treni Tanzania. Nazo ajali za moto zilipamba moto kila mahali huku hali ya kikosi cha zimamoto katika jiji la Dar es Salaam ikiwa ni ya kukatisha tamaa kabisa kutokana na uduni wa vifaa na pato.

Kwa upande wa sekta ya benki, mambo yalikuwa ya kutia matumaini kutokana na baadhi ya benki kuboresha huduma kwa wateja kwa kuanzisha utaratibu wa kutumia mitambo ya kuchukulia fedha benki. Utaratibu huu mpya umesaidia sana katika kupunguza muda wa wateja wa kusubiri huduma ya kuchukua fedha. Aidha umeleta matumaini ya kupunguza tatizo la wizi kwa vile mteja wa benki anaposafiri katika mikoa ambayo benki yake inatoa huduma halazimiki kubeba mabunda ya fedha mfukoni.

Napo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, watafiti na wafundishaji wa lugha ya Kiswahili walipata matumaini mapya ya kuanza kutumia kompyuta katika shughuli zao baada ya kuanzishwa rasmi kwa mradi wa SALAMA (Swahili Language Manager). Mradi huu ambao unahusu mbinu za kikompyuta na programu za kuchambua matini na data ya lugha ya Kiswahili kwa ajili ya utafiti na ufundishaji ulizinduliwa rasmi tarehe 10 ya mwezi wa Desemba mwaka jana na Balozi wa Suomi hapa Tanzania, Mheshimiwa Jorma Paukku. Mradi wa SALAMA umeanzishwa chini ya ushirikiano baina ya Taasisi ya Masomo ya Asia na Afrika ya Chuo Kikuu cha Helsinki na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa ufupi ni hayo tu.
Kwaherini na Karibuni Tanzania.
Sewangi na Felister (Box 35110 Dar es Salaam, Tanzania).

Downage -_-

Sivujen toteutus: Joonas From (voxel(at)mbnet.fi) ja päivitys: Andrea Fichtmüller, 2007. Suomi-Tansania seura on koonnut tämän sivuston tiedot eri lähteistä eikä vastaa niiden paikkansapitävyydestä.