Koti
kuva: L. Packalen
Tarja ja Pena

Sewangi 28.5.2003:

Barua Kutoka Dar

Wapendwa wetu wa Suomi,

Pokeeni salamu za upendo kutoka Dar. Tunapenda kuwapa hongera ya kuingia katika majira ya kiangazi baada ya kipindi kigumu cha baridi na giza. Japo tuko Dar, vichwani mwetu tunawaona mkiwa wenye furaha ndani ya mavazi yenu maridadi ya majira ya kiangazi. Tunawaona watoto wenu wanaopendeza wakirukaruka huku na kule juani huku wakifyonza krimu barafu kwa raha. Tunaisikia ngoma ya muziki wa Anold Chiwalala, mtoto wa Kimambwe ikiwatumbuiza watu wa mbari zote uwanjani kwa muziki usemao ‘Haraka haraka ya nini wewe?’ Tunamuona Traute akiota jua katika bustani yake ya mapumziko kule Martinlaakso huku kahawa yake ikiwa pembeni. Hakika, tunawaona wote mkiwa katika hekaheka za majira ya kiangazi ambazo ni burudani kwa kila mmoja.

Wapendwa wetu, huku Dar maisha yapo kama kawaida. Tulikuwa katika majira ya mvua za masika. Hata hivyo, hali ya mvua mwaka huu haikuwa nzuri kabisa. Sehemu nyingi za nchi hazikupata mvua kabisa. Ukosefu huo wa mvua unaashiria kuwa hali ya chakula haitakuwa nzuri katika baadhi ya maeneo. Kwa jumla wakulima wadogowadogo ambao maisha yao hutegemea kilimo wana hofu kubwa kutokana na ukweli kwamba hawana uwezo wa kifedha wa kujinunulia chakula sokoni. Wafugaji pia wana wasiwasi juu ya mifugo yao kutokana na ukosefu mkubwa wa majani. Wakulima wengi wa mashamba makubwa wamepata hasara kubwa kutokana na mazao yao yote kukauka. Pamoja na hali hiyo ya kutisha na kukatisha tamaa, serikali imewatoa wananchi hofu ya kufa kwa njaa kwa kuwahakikishia kwamba ina uwezo wa kuagiza chakula cha kuziba upungufu utakaotokana na ukeme huo.

Wapendwa wetu, baada ya kuwajulisha hali ilivyo kwa upande wa hali ya hewa, sasa tuwapeleke katika mambo kadhaa yaliyotokea hapa kwetu kuanzia mwezi wa Januari hadi sasa.

Tukianza na jukwaa la siasa, tarehe 4-8 Februari, tulikuwa na ugeni mzito wa Rais wa Finland, Mheshimiwa Tarja Kaarina Halonen pamoja na mumewe, Dr. Pentti Arajarvi. Katika ziara hiyo, Rais Halonen pia alitembelea visiwa vya Zanzibar ambako alikuwa na mazungumzo na Rais Amani Abeid Karume. Aidha alitembelea Mbuga za wanya za Ngorongoro huko mkoani Arusha. Tarehe 6-7 Februari, Rais Halonen alihudhuria mkutano huko Arusha ambao uliandaliwa na Tume ya kuangalia Athari za Utandawazi Duniani kwa ajili ya nchi za Afrika. Tarehe 4, Februari, Dr. Penti Arjarivi alitembelea baadhi ya Idara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuzungumza na watumishi mbalimbali wa Idara hizo. Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, Rais Halonen alisisitiza kwamba sehemu kubwa ya fedha za msaada kwa Tanzania kutoka Finland itakuwa ikitolewa kwa Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO). Hii ni kutokana na imani kwamba mashirika hayo yana nafasi kubwa ya kupiga vita umaskini kwa vile yanawahusu wananchi moja kwa moja.

Tukio lingine muhimu lililojiri katika medani ya siasa ni lile la mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri ambapo Waziri wa nchi ofisi ya Waziri mkuu (Habari na Siasa) Mheshimiwa Omari Ramadhan Mapuri alipelekwa wizara ya Mambo ya Ndani na aliyekuwa waziri wa Wizara ya Mambo ya ndani, Mheshimiwa Seif Hatib, akapelekwa Ofisi ya Waziri mkuu (Habari na Siasa).

Katika jukwaa la Uchumi, Benki kuu ya Tanzania (BoT) ilibadili noti za zamani pamoja na kutoa noti mpya ya shilingi elfu mbili. Matumizi ya noti za zamani yataendelea sambamba na noti mpya hadi mwisho wa mwezi wa Septemba. Tofauti na noti za zamani ambazo zilikuwa na picha ya mtu, noti mpya zina picha ya wanyama. Noti pekee iliyobakia na picha ya mtu ni ya shilingi elfu moja ambayo itakuwa na picha ya aliyekuwa raisi wa kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere. Noti mpya ni za shilingi mia tano, elfu moja, elfu mbili, elfu tano na elfu kumi. Kwa mara ya mwisho BoT ilifanya mabadiliko makubwa ya noti mwaka 1985,

Katika uwanja wa utamaduni na burudani, tulipata pigo la kuondokewa na mwanamuziki mkongwe na mashuhuri, Mzee Juma Kilaza, ambaye alifariki dunia mwishoni mwa Januari huko Morogoro kutokana na matatizo ya Moyo. Mzee Kilaza alikuwa mmoja wa wanamuziki mahiri katika miaka ya 1960 na 1970 akiwa katika bendi ya Cuban Marimba. Mzee Kilaza alitumia fani ya muziki kuitukuza na kuisifia nchi yake Tanzania na hasa nyumbani kwake Morogoro. Kwa mfano, katika moja ya miziki yake ya kuisifia Morogoro, Juma kilaza alisikika akiimba hivyi:

Hoye hoye Morogoro hoyee Morogoro
Hoye hoye Morogoro kwa maendeleo Moro hoyee
Hoye hoye Morogoro kwa muziki Moro hoyee
Hoye hoye Morogoro kwa mpira Moro hoyee
Hata niwe mbali na Moro nakumbuka Moro hoyee
Nakumbuka Kisangani na Midizini Moro Hoyee.

Aidha Mzee Kilaza alitumia fani ya muziki kuzungumzia mambo mbalimbali kama vile umuhimu wa kazi katika kulinda na kudumisha uhuru wa Mtanzania, manjonjo na madhila ya mapenzi, uadilifu na maswala mengine ya maisha.

Kwa upande wa Sheria, tulipata pia pigo kubwa kwa kuondokewa na Mzee wetu, Francis Nyalali, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania. Mzee Nyalali (68) alifariki tarehe 3 Aprili baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kansa. Alizikwa tarehe 6 Aprili katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam. Mzee Nyalali alistaafu kwa heshima kutokana na uadilifu wake. Hadi kustaafu, mzee Nyalali alikuwa ameweka rekodi ya kukaa katika wadhifa wa Jaji Mkuu kuliko mtu mwingine yeyote katika nchi za Jumuia ya Madola. Yeye ndiye aliyeongoza tume iliyokuwa ikijulikana kama Tume ya Nyalali ambayo ilipelekea kuanzishwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi Tanzania.

Wapendwa wetu wa Suomi tunapenda kumaliza barua hii yetu kwa kumshukuru sana Bwana Leif kwa kututembelea nyumbani kwetu Mbezi Msigani akiwa na rafiki yake aitwaye Ville. Tulikaa pamoja nyumbani kwetu tukizungumza na kufurahi kwa karibu masaa manne . Tunachukua nafasi hii kuwakaribisha wengine pia nyumbani kwetu pale watakapofika hapa Dar.

Tunawatakia Maisha ya furaha katika majira haya ya kiangazi.

Sewangi & Felister
Box 3511 Dar es Salaam
Puh. 0744 821137

Downage -_-

Sivujen toteutus: Joonas From (voxel(at)mbnet.fi) ja päivitys: Andrea Fichtmüller, 2007. Suomi-Tansania seura on koonnut tämän sivuston tiedot eri lähteistä eikä vastaa niiden paikkansapitävyydestä.