Koti
kuva: L. Packalen
Ukimwi

Sewangi 28.1.2004:

Wapendwa Wana wa Suomi, ndugu zetu na marafiki wote, tunachukua tena wasaa huu kukusalimuni na kukutakieni mwaka mpya wa mafanikio. Pia twapenda kuwafahamisha kuwa sisi huku kwetu Tanzania hatujambo kabisa.

Tunajua kuwa sasa hivi nyote mko katika matumaini makubwa ya kuingia tena katika majira ya kiangazi baada ya na kipindi kirefu cha baridi na giza. Vivyo hivyo nasi hapa tupo katika matumaini makubwa ya kuingia tena katika kipindi cha mvua za masika baada ya kuteseka na kusota katika ukame, jua kali na joto la kutisha.

Wapendwa wetu, yako mambo mengi ambayo yamekuwa yakitokea huku kwetu ambayo tunadhani ni vyema tukawamegea japo kiduchu.

Tuanze hali ya hewa. Hakika mambo hayakuwa mazuri kabisa kwa sehemu kubwa ya nchi. Katika baadhi ya mikoa kama vile Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Singida, Tabora Dodoma, Manyara, Mtwara na Arusha, jua lilikuwa kali kiasi kwamba ardhi iliwaka moto, maji na majani vilikauka. Wakulima hawakuambulia chochote mashambani mwao. Kina mama walionekana wakitangatanga huku na kule wakiwa na ndoo mikononi wakitafuta maji. Wafugaji walikata tamaa baada ya kuona ng’ombe wao wakila vumbi. Hali ya chakula na matunda ikawa mbaya kabisa. Bei ya sembe ikachupa kutoka shilingi 200 hadi shilingi 550. Mchele nao ukaruka toka shilingi mia 300 hadi mia 800. La kusikitisha zaidi ni kwamba wananchi wengi wenye kipato cha chini hawana uwezo wa kugharamia bidhaa ghali kiasi hiki. Kwa kuona hivyo, Serikali ilijitahidi kupeleka chakula katika maeneo yaliyozidiwa ambapo ama kilitolewa bure au kiliuzwa kwa bei ya chini kabisa ya hadi shilingi 50 kwa kilo.

Jambo la kufurahisha ni kwamba sasa hivi mvua zimeanza kunyesha karibu nchi nzima na ardhi yote tayari ni kijani kibichi tena. Ni matumaini ya walio wengi kuwa adha ya upungufu wa chakula itatoweka ifikapo mwezi wa Julai.

Kwa upande wa uchumi, habari zinazoendelea kutawala ni zile za kuvutia wawekezaji, hasa wageni, katika kuchimbua rasilimali ghafi hususani madini. Kutokana msisitizo mkubwa wa uwekezaji kuwekwa kwa wageni, neno ya ‘ugenishaji wa uchimi’ limekuwa ikitumiwa na baadhi ya Watanzania badala ya lile la uwekezaji. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bwana, Samwel Sitta, Tanzania, kama ilivyo Uganda, imeongoza katika mwaka 2003 katika kuvutia mitaji toka nje. Hata hivyo, pamoja na kasi ya ugenishaji, bado hali ya maisha ya Watanzania hasa wakulima vijijini inazidi kuzorota kabisa. Bei ya mazao makuu, kama vile kahawa imeendelea kudidimia kabisa. Kwa sasa hivi kilo moja ya Kahawa inauzwa shilingi mia 300 hadi 400 ( EURO 0.25). Kutokana na hali hiyo baadhi ya wakulima wametelekeza kabisa zao la kahawa. Kuzorota kwa maisha huko vijijini kumesababisha vijana wengi kukimbilia mijini hasa katika jiji la Dar es Salama ambako hushinda wakizurura bila kazi maalum.

Kwa upande wa siasa, hivi karibuni Watanzania walipokea kauli rasmi ya Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba kuwa hana mpango wa kugombea madaraka yoyote serikalini, yakiwemo yale ya urais, kwa vile anaamini kuwa nafasi za uongozi ni vyema zikashikwa na watu wenye umri mdogo hasa vijana. Alisema kuwa yeye sasa umri wake haumruhusu kugombea tena madaraka serikalini na akawaomba wazee wenzake watafakari hilo pia. Mpaka sasa ni mzee mmoja tu ambaye ameungana na busara hii ya Mheshimiwa Warioba na kueleza rasmi kuwa hana mpango wa kugombea madaraka serikalini. Mzee huyo ni Mheshimiwa Bob Makani, mwenyekiti wa chama cha CHADEMA. Wazee wengine bado wanatafakari na bila shaka watatoa kauli zao rasmi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2005.

Tukiwa bado kwenye uwanja wa siasa, tarehe 12/1/04, kama kawaida ilikuwa siku ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar. Kile kilichovutia na kufurahisha Watanzania wengi kilikuwa ni kule kushiriki kwa mara ya kwanza kwa chama cha CUF katika sherehe hizo. Chama cha CUF ambacho kimekuwa kikidai kutoyatambua mapinduzi, kilishiriki kikamilifu katika sherehe hizo ikiwa ni ishara ya kumalizika kwa uhasama wa kisiasa baina ya chama hicho na chama tawala cha CCM.

Kati ya Novemba 9 hadi Desemba 16/2003, Raisi wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin W. Mkapa alilazwa katika hospitali ya Hirslanden huko Zurich kwa matibabu ambapo alifanyiwa upasuaji wa kutibu sehemu ya mfupa inayounganisha mguu wake wa kushoto na nyonga. Katika kipindi hicho Watanzania wengi walimtumia Raisi wao salamu za pole na za kumtakia nafuu. Aidha walifanya sala na dua mbalimbali kwa mujibu wa imani zao. Naye Raisi alipopata nafuu na kurejea nyumbani aliwashukuru Watanzania kwa kumuombea wakati wa ugonjwa wake. Wakati akiwashukuru, Raisi aliwaambia Watanzania kuwa ugonjwa wake ulikuwa na mafundisho mengi kwa Watanzania. Kwa mujibu wa Rais, funzo mojawapo ni kuwa binadamu wa hadhi yoyote anaweza kuugua kwa wakati wowote na funzo la lingine ni kuwa ni vyema kutodharau dalili za ugonjwa wowote ule na kutobeza kupumzika.

Kwa upande wa Afya, habari za ugonjwa wa UKIMWI ziliendelea kutawala. Taarifa mojawapo muhimu ilikuwa ni ile ya Dawa za kupunguza makali ya UKIMWI kuanza kutengenezwa Tanzania. Utengenezaji wa dawa hizo utafanywa na kampuni ya Tanzania Pharmaceutical Industires Lited ikishirikiana na mtaalamu wa dawa toka Thailand, Dkt. Krisana Kraisintu. Tanzania inakuwa nchi ya tatu barani Afrika kusaidiwa na Dkt. Kraisintu katika utengenezaji wa dawa hizi. Nchi nyingine ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Eritrea.

Habari nyingine za UKIMWI zilihusu hali ilivyo mbaya katika wilaya ya Kibaha mkoani Pwani kwa upande wa idadi ya watoto wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Wilaya hiyo ambayo ndiyo iliyoathirika zaidi katika mkoa wa Pwani ina jumla ya yatima 4,000 ambao wazazi wao wote wamepoteza maisha kutokana na UKIMWI.

Kwa jumla hali ya ugonjwa wa UKIMWI bado ni mbaya na hivi karibuni Waziri Mkuu, Mheshimiwa F. Sumaye alisisitiza sana juu ya matumizi ya kondomu katika mchezo wa ngono. Waziri alifikia kiasi cha kuwaambia wananchi kuwa yeye binafsi huwapatia kondomu watoto wake wanaosoma shule ili waweze kujikinga pale watakaposhindwa kabisa kujizuia dhidi ya kimuhemuhe cha ngono. Kwa jumla viongozi wa dini mbalimbali, kwa nguvu zao zote, wamekuwa mstari wa mbele katika kupiga vita matumizi ya kondomu. Hata hivyo, kampeni za kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kondomu zinaendelea kupitia vyombo mbalimbali vya uma na hivi sasa upatikanaji wa kondomu hauna matatizo kwani zipo karibu sehemu zote na vijana wengi wanaonekana kuzichangamkia bila haya tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

Kwa upande wa maswala ya Mazingira, habari iliyovuta wengi ilikuwa ni juu ya kuvuliwa kwa samaki aina ya nguva huko katika Kisiwa cha Mafya. Nguvu huyo dume aliyevuliwa alikuwa na uzito wa kilo 157 na urefu wa mita 3. Samaki huyo amehifadhiwa katika kiwanda cha kusindika samaki cha Tan Pester kwa ajili ya shughuli za utafiti wa viumbe wa baharini. Kwa mara ya mwisho samaki wa aina ya nguvu alivuliwa huko Mafya mwaka 1981.

Kuhusu mikasa na vifo, habari iliyokuna vichwa vya wengi ilikuwa ile ya kufariki kwa Dkt. Hukwe Sawoze, msanii na mwalimu wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo. Dkt Sawoze alikuwa gwiji la muziki wa jadi hasa katika kuzicharaza ala za marimba, zeze na filimbi. Vilevile alikuwa mwimbaji hodari sana. Dkt Sawoze ambaye alizaliwa 1940 alifariki tarehe 30/12/2003 asubuhi huko nyumbani kwake Bagamoyo.

Msiba mwingine mkubwa ulikuwa ule wa aliyekuwa mkuu wa majeshi ya ulinzi Jenerali Abdallah Twalipo. Mzee Twalipo alifariki tarehe 4/1/04 akiwa na umri wa miaka 74.

Kwa upande wa mikasa, tarehe 23/01/04, ulizuka moto mkubwa kabisa sehemu ya Ubungo, Dar es Salaam, katika matanki ya mafuta ya kituo cha kuzalishia umeme wa gesi cha Shirika la Umeme nchini (TANESCO). Moto huo ambao ulianza majira ya saa 12 jioni ulikuwa mkubwa kiasi kwamba moshi wake ulitanda sehemu kubwa ya anga hapa jijini. Vyombo mbalimbali vya kuzima moto vilifanya kazi kubwa, takribani usiku kucha, ya kuuzima moto huo. Kwa bahati mbaya katika mapambano hayo dereva mmoja wa kikosi cha zima moto alipoteza maisha.

Wapendwa wetu wa Suomi tunamalizia barua hii kuwafahamisha kuwa wakati nikiandika barua hii nilikuwa na wageni wawili kutoka huko Suomi walionitembelea ofisini kwangu. Wageni hao ni Anold Chiwalala pamoja na rafiki yake Topi ambaye amenieleza kuwa hii ndiyo mara yake ya kwanza kufika Tanzania na Afrika tangu azaliwe. Topi ambaye anasema amevutiwa sana na mandhari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na chakula kitamu cha Kitanzania, yuko njiani, pamoja na Chiwalala, kuelekea Bagamoyo na hatimaye Zanzibar.

Nanyi wengine tunawakaribisha sana Tanzania.

Ni sisi

Sewangi & Felister
Box 35110 DSM
Puh. 0744-821137

Downage -_-

Sivujen toteutus: Joonas From (voxel(at)mbnet.fi) ja päivitys: Andrea Fichtmüller, 2007. Suomi-Tansania seura on koonnut tämän sivuston tiedot eri lähteistä eikä vastaa niiden paikkansapitävyydestä.