Koti
kuva: L. Packalen
AU

Sewangi 27.7.2004

27.7.2004 Wapendwa, ndugu zetu na marafiki wote wa Suomi, twakusalimuni nyote tukitumai kuwa mwaendelea vyema na shamrashamra za majira ya kiangazi. Huku kwetu Tanzania hatujambo kabisa.

Tunajua kuwa sasa hivi nyote mko katika shamrashamra za majira ya kiangazi ambazo huandamana na mambo mengi, tangu michezo hadi kuchuma matunda matamu ya Suomi, kama vile mustikka na mansikka. Hapa kwetu tunakaribia ukingoni mwa majira ya baridi. Mwaka huu kumekuwa na baridi kali kidogo hasa katika sehemu za miinuko kama kule nyanda za juu kusini na katika maeneo ya milima Meru na Kiliman-jaro. Hata pande za pwani kama vile hapa Dar es Salaam kuna baridi hasa wakati wa usiku kiasi cha kuwafanya watu wajishughulishe na makoti.

Wapendwa wetu, hakiki ni muda tangu tulipowatumia barua yetu ya mwisho. Mambo mengi yametokea huku kwetu kama ilivyo huko kwenu. Hivyo basi kama ilivyo ada yetu tungependa kukumegeeni japo kiduchu katika hayo mengi tukitaraji kuwa yatakuwa na manufaa ya hapa na pale kwa upande wenu.

Tuanze vijambo vya uchumi. Wataala-mu wa Taasisi ya Kimataifa ya Deloitte Touche, ambayo hujishughulisha na utoaji wa ushauri na maswala ya kiuchumi na fedha wamewapa watan-zania matumaini mapya ya kuboreka tena kwa uchumi baada ya kipindi cha ukame hapo mwaka jana, ambacho kilisababisha kuyumba kidogo kwa uchumi.

Pamoja na kuwa hata mwaka huu hali ya hewa haikuwa nzuri sana, wataalamu hao wanadai kuwa uchumi utaboreka kwa sababu ya kasi ya kukua kwa miundo mbinu, hasa barabara. Sasa hivi ujenzi wa barabara za lami na madaraja ya kudumu umepamba moto nchi nzima. Inatarajiwa kwamba eneo kubwa la nchi litaunganishwa kwa barabara za lami katika kipindi kufupi kijacho kutokana na mipango hiyo kabambe ya ujenzi wa barabara.

Hivi karibuni inatarajiwa kuwa ujenzi wa barabara ya lami ya kilometa 487 toka Dodoma hadi Kigoma utaanza. Tayari ujenzi wa barabara ya lami toka Dodoma hadi Mwanza unaendelea sambamba na ule wa barabara ya lami ya Kibiti hadi Lindi. Aidha ujenzi wa madaraja ya kudumu katika barabara ya Mbeya hadi Sumbawanga unaendelea kwa kasi.

Sekta nyingine inayotoa matumaini ya kuimarika kwa uchumi ni ile ya umeme ambayo hivi karibuni imepata msukumo mpya baada ya kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia gesi ya asili. Gesi hiyo ambayo huchimbwa huko Songosongo Kilwa, husafirishwa katika mabomba hadi katika kituo cha TANESCO cha Ubungo ambako hutumika kuzalishia umeme. Uzalishaji ulianza mapema mwezi wa saba mwaka huu. Hata hivyo, pamoja na matumaini haya mapya ya kuimarika kwa sekta ya umeme, bado kwa watumiaji wa umeme majumbani mambo sio mazuri sana kwani mwezi Juni walishuhudia ongezeko kubwa la bei ya umeme wa majumbani.

Kwa mujibu wa shirika la umeme, TANESCO, ongezeko hilo limetokana na kushuka kwa thamani ya shilingi na kupanda kwa bei ya mafuta. Kwa vyovyote vile ongezeko hili ni mzigo zaidi kwa watumiaji umeme majumbani hasa kwa vile kipato chao hakipimwi kwa thamani ya dola wala bei ya mafuta. Wateja wengi wa majumbani walikuwa na matumaini kwamba baada ya kuanza kwa uzalishaji wa umeme wa gesi ya Songosongo bei ya umeme ingepungua. Hata hivyo matumaini hayo yameyeyuka baada ya kuambiwa na Shirika husika kuwa hilo halitatokea kwa sasa.

Kama ilivyo ada, mwezi Juni tuliso-mewa bajeti ya mwaka mpya wa fedha. Bajeti ilikuwa na mambo mengi lakini yaliyovuta zaidi masikio ya wengi yaliuwa ni kuondolewa kwa ushuru wa kuingiza dawa za binadamu na vyan-darua vya mbu. Kwa wakulima, lililowafurahisha sana ni kuondolewa kwa ushuru kwa vifaa vya kilimo, uvuvi na pembejeo. Aidha wengi walifurahi-shwa na kupunguzwa kwa ada ya sekondari za serikali za kutwa kutoka shilingi elfu arobaini hadi shilingi elfu ishirini kwa mwaka.

Tukiachilia mbali maswala ya uchumi ambayo kwa hakika ndiyo maisha yenyewe, yapo mambo mengine ya hapa na pale yaliyojiri hapa. Katika hayo lipo lile la adhabu ya kifungo cha maisha iliyotolewa kwa Msanii maarufu wa muziki wa dansi, Nguza Viking ‘Babu Seya’ pamoja na wana-we watatu. Hukumu hiyo iliwaangu-kiwa baada ya kutiwa hatiani na mkono wa sheria kwa kosa la kuwafanyia ‘mchezo mchafu’ wavulana wadogo wa shule ya msingi.

Pamoja na ubaya wa kosa lililosaba-bisha hukumu hiyo, watu wengi waliohudhuria mahakamani siku hiyo ya hukumu, hususan wapenzi wa gwiji hilo la muziki na wanawe, walishindwa kuyazuia macho yao yasibubujike michozi na midomo yao isiachame na kutema udelele kwa uchungu pale walipoona Nguza na wanawe, wakie-lekea kwenye karandinga la polisi tayari kwa safari ya kumalizia maisha yao huko gerezani. Pamoja na hukumu hiyo kali, wahukumiwa wote waliru-husiwa kukata rufaa kama hawakuri-dhika na uamuzi wa mahakama.

Jambo lingine lililotokea na la kuche-kesha kidogo ni pale waganga kadhaa wa kienyeji walipobambwa wakisindika bunduki kwa ajili ya vitendo vya ujambazi. Staili hiyo mpya ya majambazi ya kutumia waganga wa kienyeji, ambayo imeenea sana siku hizi hapa Bongo, ilitumbukia nyongo pale waganga wawili waliponaswa na polisi wakiwa katika harakati za kuisindika bunduki tayari kwa kutumika katika vitendo vya ujambazi. Baada ya waganga hao kupata kibano cha polisi walikiri kuwa walikuwa na kamchezo hako ka kuwasaidia majambazi kwa ndumba. Kwa sasa hivi magwiji hao wa ndumba wako rumande wakisubiri mkono wa sheria utende kazi yake juu ya ubaradhuli wao.

Yako mambo kadhaa ya kusikitisha yaliyotufika hapa. Mojawapo ni lile la kufariki ghafla kwa Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM) wakati akiwa huko Dodoma katika vikao vya Bunge. Kwa mujibu wa habari za magazetini kifo cha Mbunge huyo, Mheshimiwa Aintemule Mwalyengo, kilitokana na kiharusi. Wakati tunaka-milisha kuandika waraka huu, tumepo-kea habari za kifo cha ghafla cha mbunge mwingine huko Dodoma. Mbunge huyo (CCM) ni James Kasapira (maarufu kama Komredi) wa Jimbo la Ulanga Mashariki mkoani Morogoro. Kifo cha Mbunge huyu kilitokea ghafla akiwa usingizini huko Dodoma. Kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo Hayati Kasapira aliwahi kusoma huko Finland mwaka 1999 ambapo alichukua mafunzo ya fani ya utunzaji wa fedha ngazi ya cheti. Bila shaka wakati wa masomo yake huko Finland alikutana na baadhi ya watan-zania wanaoishi huko. Kwa wale mliomfahamu, basi mwenzetu hatunaye tena katika maisha haya tuyajuayo.

Tukio lingine la kusikitisha ni lile la kupinduka kwa gari la Makongoro Nyerere, Mbunge wa kuteuliwa (CCM). Ajali hiyo ilitokea huko katika eneo la Maseyu Morogoro na kumsa-babishia Mheshimiwa Makongoro majeraha ambayo anaendelea kuyau-guza katika Hospitali ya Muhimbili. Makongoro alifikwa na ajili hiyo akis-afiri toka Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Basi ndugu zetu kwa leo tukomee hapa hadi tutakapojaliwa tena.

Sewangis

Ni sisi,
Sewangi
& Felister
Box 35110 DSM
Puh. 0744-821137

Downage -_-

Sivujen toteutus: Joonas From (voxel(at)mbnet.fi) ja päivitys: Andrea Fichtmüller, 2007. Suomi-Tansania seura on koonnut tämän sivuston tiedot eri lähteistä eikä vastaa niiden paikkansapitävyydestä.