Koti
kuva: L. Packalen
Kahawa

Sewangi 19.2.2002

Barua kutoka Dar

Wapendwa wetu wa Suomi

Twawasalimu kutoka Dar tukitumaini kuwa mliunza mwaka 2002 kwa furaha na matumaini.

Wapendwa, twaamini kuwa wapo ambao hatukupata nafasi ya kuwapa mkono wa kwa heri, kwa hali hiyo tungependa kutumia barua hii kuwajulisha rasmi kuwa sisi tulirejea nyumbani Tanzania mwishoni mwa mwaka jana baada ya kumaliza masomo yetu.

Wapendwa, safari yetu ya kurejea nyumbani ilikuwa salama. Hata hivyo, tulipoingia jinini Dar, tulishtushwa na mambo mengi kiasi kwamba tulijiona wageni katika nchi yetu wenyewe.

Mshtuko wa kwanza tulioupata ni wa mabadiliko ya ghafla ya hali ya hewa. Tulipotoka Helsiniki, hali ya hewa ilikuwa baridi sana na theluji nyingi. Hivyo ilitubidi tuvae mavazi rasmi ya baridi. Tulipoingia Dar, tulikuta hali ya joto sana kiasi kwamba tulitokwa jasho kama vile tuko ndani ya Sauna. Hapo tulijua rasimi kwamba tumerejea nyumbani.

Mshtuko wa pili ulitupata pale tulipofika katika barabara ya Morogoro pale Ubongo. Barabara hii haikuwa ile nyembamba na yenye mashimo mengi ambayo tuliiacha tulipoondoka miaka mitano iliyopita. Hii ilikuwa barabara kubwa ya njia nne ambayo ilipambwa na taa za barabarani zilizowaka kwa rangi tofautitofauti za kupendeza.

Mshtuko wa tatu ulitupata siku ya pili tulipokwenda sokoni. Tulikuta vyakula vingi pamoja na matunda mengi yakiwemo maembe, mapapai, ndizi mbivu, machenza, mananasi, na machungwa. Vyakula hivo pamoja na matunda vilitoka shambani moja kwa moja hivyo vilikuwa na ule utamu na ladha ya asili kabisa. Basi tulinunua matunda yale kwa wingi kiasi kwamba watu waliokuwa karibu pale sokoni walitushangaa kwa jambo lile.

Mshtuko wa nne tuliushuhudia pale tulipofika kijijini kwetu Ugweno kuwatembelea wazazi na jamaa. Hali ya maisha ya watu kijijini ilkuwa imeshuka sana ikilinganishwa na ile tuliyokuwa tumeiacha miaka mitano iliyopita. Shule nyingi za Sekondarai za kulipia hazina wanafunzi kwa vile wazazi hawana ada. Hali ya ujenzi wa nyumba za kisasa imeshuka sana. Hali ya matibabu ni duni kabisa. Chanzo cha haya yote ni hiki hapa: Miaka mitano iliyopita, kilo moja ya kahawa ilikuwa ikiuzwa kwa shilingi elfu moja na mia tano (sawa na dola 2.5 kwa wakati huo). Hivi sasa kilo moja ya kahawa inauzwa shilingi mia tatu (sawa na dola 0.3 kwa wakati huu) Wakati huo huo mfuko mmoja wa saruji ambao ulikuwa ukiuzwa shilingi elfu tatu miaka mitano iliyopita, sasa hivi unauzwa shilingi elfu saba na mia nane. Hali hii ya kushuka sana kwa bei za mazao na kupanda sana kwa bei za bidhaa za viwandani imeyafanya maisha ya wakulima wa Tanzania, kwa jumla, yawe duni kiasi cha kutisha. Hali inakuwa mbaya zaidi kwa vile, pamoja na kuwa pato la mkulima limepungua sana, mkulima huyohuyo anapaswa agharamie gharama zote za mahitaji yake ya msingi, ikiwa ni pamoja na matibabu na shule kwa watoto wake , na alipe kodi ya Serikali za mitaa.

Kushuka kwa bei ya zao la kahawa kumeadhiri sana hali ya uzalishaji wa kahawa. Wakulima wengi wameshindwa kununua dawa za wadudu wa kahawa. Bei ya dawa hizo ni ya juu sana ikilinganishwa na bei ya kahawa. Kahawa zimeshambuliwa na wadudu kiasi cha kuzifanya zionekane kama vichaka vya miti. Uduni huu wa mikahawa umezidi kudidimiza pato la mkulima kwa vile umepunguza sana kiwango cha kahawa inayozalishwa.

Pamoja na mishtuko hiyo tuliyoipata baada ya kuishi ugenini kwa miaka mitano, yapo mambo mengine machache yaliyotokea hapa nyumbani ambayo tumeyashuhudia hivi karibuni:

Jambo la kwanza ni kuondolewa rasmi kwa ada ya elimu ya msingi. Kuanzia mwaka huu, wanafunzi wote wa shule za msingi hawatalipa ada ya aina yoyote. Hali hiyo imepelekea kufurika kwa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza katika mashule, hasa katika jiji la Dar es Salaam. Zipo shule ambazo idadi ya wanafunzi waliojitokeza kuanza darasa la kwanza ni mara tano ya uwezo wa shule. Kutokana na hali hii, imebidi shule za msingi za jijini zianzishe utaratibu wa madarasa ya asubuhi na ya jioni. Pamoja na kuanzishwa kwa utaratibu huu, bado kuna tatizo kubwa la majengo na vifaa kiasi kwamba wanafunzi wengi hulindikana sana katika darasa moja huku wakiwa wamekaa chini.

Jambo lingine lilotokea hapa, ambalo ni la kuhuzunisha kidogo, ni lile la moto kuteketeza jengo la kisasa la ukumbi wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo. Tukio hili lilitokea tarehe 31/ 1/ 2002, majira ya asubuhi. Kwa mujibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho, chanzo cha moto huo huenda ikawa ni hitilafu ya umeme. Jengo hilo lililoungua lilikuwa na ofisi kubwa mbili na ndogo moja, kumbi kubwa mbili na ndogo moja za maonyesho. Aidha lilikuwa na ukumbi wa wasanii wa kubadilisha nguo. Vifaa mbalimbali vya mamilioni ya fedha viliteketea ndani ya jengo hilo. Hasara za moto huo zimekuwa kubwa zaidi kwa vile juhudi za kuuzima moto huo zilishindikana kutokana na kutokuweko kwa zimamoto na vifaa vya kuzimia moto hapo Chuoni na katika mji wa Bagamoyo. Hata hivyo, moto huo haukumjeruhi mtu yeyote.

Jambo lingine lililotokea na la kufurahisha kwa Watanzania wengi ni kumalizika rasmi kwa uhasama baina ya vyama vya siasa vya CCM na CUF. Hali hii ilitokana na maafikiano yaliyofikiwa na viongozi wa juu wa vyama hivyo. Kutokana na maafikiano hayo, chama cha CUF sasa kinaitambua rasmi serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kipo tayari kufanya kazi na serikali hili. Aidha rais Mkapa amemteua mbunge mmoja kutoka katika chama hicho cha CUF na kukamilisha jumla ya wabunge 10 ambao anaruhusiwa kuwateua kikatiba. Wabunge wengine tisa aliowateua wanatoka chama cha CCM.

Jambo la mwisho ambalo limetokea na kuwakera watu wengi hivi karibuni kabisa ni lile la serikali kumnyimwa Bwana Jenerali Ulimwengu uraia wa Tanzania. Kulingana na magazeti ya hapa, sababu hasa za kunyimwa uraia hazikuelezwa. Bwana Ulimwengu ambaye amekulia hapa Tanzania na kushika nyadhifa mbalimbali za kisiasa aliomba uraia huo baada ya kutakiwa afanye hivyo na serikali ya Tanzania. Kutokana na tukio hilo la kunyimwa uraia, vikundi mbalimbali vya wanaharakati, ukiwemo umoja wa wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, vimeiomba serikali ilitazame tena upya swala hilo ili ama impatie Bwana Ulimwengu uraia au imueleza waziwazi sababu za kumnyimba uraia huo.

Wapendwa, kwa haya machache, tunapenda kuwaaga tukisema:

Udumu urafiki wa Watanzania na Wasuomi

Ni sisi

Sewangi na Felister
Box 35110
Dar es Salaam.

Downage -_-

Sivujen toteutus: Joonas From (voxel(at)mbnet.fi) ja päivitys: Andrea Fichtmüller, 2007. Suomi-Tansania seura on koonnut tämän sivuston tiedot eri lähteistä eikä vastaa niiden paikkansapitävyydestä.